FAHAMU KUHUSU HOMA YA INI

Posted on: November 21st, 2019

UGONJWA WA HOMA YA INI NA MAMBO MUHIMU KUFAHAMU

 

 

Ini ni kiungo muhimu sana ndani ya miili yetu, hufanya kazi zaidi ya 500 ; moja ya kazi ni kuchuja na kuondoa sumu kutoka kwenye damu.

Kutokana na sababu mbalimbali kama pombe iliyopita kiasi, sumu kwenye damu au maambukizi; ini hupata shida na kuvimba na kushindwa kufanya kazi vizuri. Hii hali huitwa HOMA YA INI au HEPATITIS.

Katika maeneo yetu, bara la Afrika maambukizi ya virusi wa Homa ya ini ndio sababu kuu ya shida kwenye ini. Virusi vya Homa ya ini vipo vya aina 5 (A,B,C,D,E).

Aina mbili za virusi (B na C ) ndio sababu kuu za ugonjwa wa homa ya ini na husambaa kupitia damu na majimaji ya mwili.

Homa ya ini ni sawa janga linaloua kimya kimya kulingana na takwimu za vifo za dunia inakadiriwa Kirusi cha homa ya ini aina ya B pekee huua watu 600,000 hivi kila mwaka.

Kwa wastani zaidi ya watu bilioni mbili, yaani, asilimia 33 hivi ya watu wote ulimwenguni, wameambukizwa virusi vya HBV, na wengi wao hupona baada ya miezi michache. Watu milioni 350 hivi huendelea kuwa na virusi hivyo mwilini, wengi huishi bila dalili na kuendelea kuambukiza watu wengine

 

NAMNA GANI UNAWEZA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA HOMA YA INI (B NA C)…….?

Virusi vya homa ya ini B na C husambaa kupitia damu, shahawa au maji maji mengine ya mwili.

Virusi hivi vina uwezo wa kusambaa na kuambukiza mtu mara 100 zaidi ya virusi vya UKIMWI.

Njia hizi husambaza virusi hivi vya homa ya ini..:

Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Mama aliye na maambukizi ya Hepatitis B kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua, iwapo hamna juhudi za kitiba za kuzuia maambukizi kuna uwezekano hadi asilimia 90 kwa mama kumuambukiza mtoto.

 

Kufanya mapenzi na mtu mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini

Kuchangia vifaa vyenye ncha Kali kama sindano hasa kwa watumia madawa ya kulevya au wachora tattoo, miswaki

Kuongezewa damu ambayo ina maambukizi ya homa ya ini.


Virusi vya homa ya ini vinaweza ishi nje ya mwili kwa muda mrefu…

Tafiti zinaonyesha virusi vya homa ya ini vinaweza ishi nje ya mwili hadi kwa muda wa siku 7, bado vikiwa na uwezo wa kuambukiza mtu. Tafiti zimeonyesha hata iliyokauka huwa na uwezo wa kuambukiza virusi hivi.

 

 

 

 

NB : Iwapo kuna damu imemwagika inatakiwa isafishwe na chlorine au spirit ili kuua virusi 

NANI YUPO KATIKA HATARI ZAIDI YA KUPATA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA HOMA YA INI?  

*  Watoto wachanga waliozaliwa na mama aliye na maambukizi ya virusi vya homa ya ini 

 *  Watu wanaofanya biashara ya ngono

*   Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao

*   Watu wanaojidunga dawa za kulevya

*   Mtu mwenye mpenzi ambaye anaishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini

*   Wafanyakazi wa sekta ya Afya

*   Watu wa familia wenye ndugu anayeishi na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini

*    Wagonjwa wa figo wanaotumia huduma za kusafisha damu (dialysis)

  

UGONJWA WA VIRUSI VYA HOMA YA INI HUJA NA DALILI MBALIMBALI…..

   

Dalili za muda mfupi (acute hepatitis)

   

➡️ Dalili hizi za mwanzo hutokea ndani ya miezi 6 baada kuambukizwa virusi vya homa ya ini, hutokea kwa baadhi ya watu hazitokei kwa kila mtu.

Mgonjwa mwenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini hujiskia kuumwa


* Hupoteza hamu ya kula

* Kichefuchefu na kutapika

* Mwili kuumaMkojo kuwa na rangi iliyokolea kama Coca-Cola

* Kupata manjano kwenye macho, vinganja vya mikono/kucha au mwili      mzima.


 

Kuna kundi dogo la wagonjwa wa homa ya ini hupata ugonjwa mkali wa ini na kusababisha ini kushindwa kabisa kufanya kazi pia huweza kusababisha kifo. Hii hatua huitwa “fulminant liver failure”.

 

Maambukizi ya kudumu ya virusi vya Homa ya ini (chronic hepatitis)

Watu wenye maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini mara nyingi huwa hawana dalili, kadri muda unavyoenda virusi husababisha ini kusinyaa (cirrhosis) na kushindwa kufanya kazi vyema.

  

 

  


Pia Maambukizi ya virusi vya homa ya ini huchangia pia kupata Saratani ya ini.

 

 

Kwa nini ni muhimu kupima ili kujua kama una maambukizi ya virusi vya homa ya ini? ….

Watu wengi huishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini bila kufahamu. Kwa kawaida katika kipindi fulani cha maisha mtu 1 kati ya watu 3 huambukizwa virusi vya homa ya ini. Baada ya kuambukizwa, kuna kundi la watu hubaki na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini ambayo huwa hayana dalili yoyote na kuendelea kuua ini kimyakimya. Dalili huja kuonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa. Huonekana wakati tayari ini limenyauka au lina kansa.

Hivyo Mtu aliye na maambukizi ya kudumu ya virusi vya homa ya ini aina B akianza matibabu mapema, anaweza kuzuia ini lake lisiharibike sana. Pia kwa wenye maambukizi ya virusi aina C matibabu ya dawa wiki 12 humaliza virusi vyote.

 

NANI ANAHITAJI KUPIMWA MAAMBUKIZI YA HOMA YA INI?  

 

 

Watu kutoka makundi yafuatayo ni sharti kupimwa kama wana maambukizi ya virusi wa homa ya ini……  

Watu wanaoishi kwenye maeneo yenye maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa zaidi ya asilimia 2. -Tanzania ni moja ya nchi zenye kiwango cha maambukizi ya virusi vya homa ya ini kwa wastani wa 5% hivyo watanzania wote ni muhimu kupima

* Watu wote wanaotumia dawa za kulevya na kujidunga

* Wafanyakazi katika sekta ya afya

* Watu wote wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI

* Watu wote ndani ya familia wanaoshi na ndugu aliyeambukizwa virusi vya homa ya ini

* Watu wote wanaotumia dawa za kufubaza kinga ya mwili (immunosuppressive therapy)

* Watu wote wenye ugonjwa wa figo wanahitaji kuanza dialysis

* Kina mama wajawazito wote

* Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao.

 

UGONJWA WA HOMA YA INI HUWA NA MATOKEO MABAYA…..

Kwa wastani watu 25 kati ya 100 walioambukizwa virusi vya homa ya ini wakiwa watoto na 15 kati ya 100 waliopata maambukizi ya kudumu ya homa ya ini baada ya utoto hufariki wakiwa na umri mdogo kwa ugonjwa wa ini (ini kushindwa kufanya kazi) au saratani ya ini.


CHANJO YA DHIDI YA VIRUSI VYA HOMA YA INI

  

 

 

Chanjo dhidi ya homa ya ini hutolewa kwa watoto wote kama ilivyo kwenye mpango wa chanjo wa Taifa, pia hutolewa kwa watu wazima ambao hawajawahi kupata chanjo.

Chanjo hutolewa kwa njia ya sindano, ambapo huwa ni sindano 3; sindano ya kwanza hutolewa baada ya kupimwa kujua kama hauna maambukizi tayari, sindano ya pili hutolewa baada ya mwezi mmoja na sindano ya 3 baada ya miezi 6.

Makundi ambayo ni lazima kupatiwa chanjo ya homa ya ini

* Watoto wote

* Watu wote wanaotumia dawa za kulevya na kujifungua

* Watu wote wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI

* Watu wote ndani ya familia wanaoshi na ndugu aliyeambukizwa virusi vya homa ya ini

* Watu wote wanaotumia dawa za kufubaza kinga ya mwili (immunosuppressive therapy)

* Wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao

* Watu wote wanaoufanya biashara ya ngono

* Watu wote ambao wana mpenzi zaidi ya mmoja ndani ya miezi 6

* Watu wenye maradhi ya kudumu ya ini

* Watu wengine wote wanahitaji KUJIKINGA dhidi ya virusi vya homa ya ini